ZFDA YAFUNGIA KIWANDA CHA KUZALISHA SANITIZER FEKI KIEMBESAMAKI

Mkuu wa Kitengo cha Vipodozi wa ZFDA Salim Hamad Kassim akiwaonyesha waandishi wa habari Dawa ya Kuoshea Mikono (SANITAIZER) ambayo haina Kiwango iliyotengenezwa na Kiwanda cha Oil Cam kilichopo Kiembesamaki, Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja.

Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imekifunga kiwanda cha kutengeneza dawa za kukosha mikono (SANITIZER) baada ya kubainika dawa hizo hazina kiwango kinachohitajika pamoja na kutokuwa na usajili rasmi.

Hatua ya kukifungia kiwanda hicho kinachojulikana kwa jina la OIL CAM kilichopo Kiembesamaki imekuja baada ya wasamaria wema kutoa taarifa kwa Mamlaka hiyo.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Mkuu wa Kitengo cha Vipodozi ZFDA Salim Hamad Kassim amesema kwa hatua ya awali wameamua kukifunga kiwanda hicho na kumpa nafasi mmiliki kufuata taratibu za usjili na kuwasilisha sampuli ya bidhaa wanayozalisha ili ifanyiwe uchunguzi katika maabara yao.

Amesema kawaida bidhaa za viwandani kabla ya kufika kwa watumiaji zinatakiwa zifanyiwe uchunguzi na zifikie kiwango cha ubora unaokubalika kulingana na muongozo  wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kuanzia asilimia 75 hatua ambayo bidhaa hiyo haikufikia.

Aliongeza kuwa walichogundua katika kiwanda hicho ni kuweka nembo bandia inayoonesha bidhaa hiyo inazalishwa nchini Marekani jambo ambalo sio kweli.

Hata hivyo amesema kukifunga kiwanda hicho ni kwa mujibu wa sheria  ambazo zimewekwa na Serikali kuu pamoja na Mamlaka husika.

Mkuu wa Kitengo cha Vipodozi alieleza kuwa kwa mujibu wa uchunguzi waliofanya katika maduka mbali mbali chupa yenye ujazo wa nusu lita inauzwa shilingi 25,000 kwa rejareja na jumla inauzwa shilingi 18,000.

Muangalizi wa Ubora na Usalama na Ufanisi wa Dawa Sokoni Nasir Salum Buheti amesema kuwa watawaagiza wenye maduka kusitisha kuuza  bidhaa za kiwanda hicho na wataendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuwa waangalifu wanaponunua bidhaa dukani.

 Aidha amesema Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar itaanzisha msako zaidi katika kipindi hichi cha mripuko wa maradhi ya corona ili kuhakikisha bidhaa zinazouzwa zinakuwa na kiwango na zimethibitishwa na Mamlaka hiyo.

Amesema ZFDA haina nia ya kumuonea mtu bali imewataka wajasiriamali wanaotengeneza sabuni za kukoshea mikono kwa ajili ya kujikinga na Corona na bidhaa nyengine wahahakishe kuwa wanafuata taratibu ili kulinda afya za watumiaji.

Mmiliki wa kiwanda hicho aliejulikana kwa jina moja tu la Mustafa hakuwepo katika maeneo ya kiwanda wakati wa ukaguzi na baadhi ya wafanyakazi wake walisema kuwa amesafiri kwenda Dar es salaam.

Loading