ZFDA YATEKETEZA TANI 183 YA BIDHAA ZILIZOHARIBIKA NA ZILIZOPITWA NA MUDA WA MATUMIZI

Wafanyakazi wa Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) wakishusha tani 183 za bidhaa zilizoharibika za mchele, unga wa ngano na tende kwa ajili ya kuteketezwa katika Jaa la Kibele, Wilaya ya Kati Mkoa Kusini Unguja.

Mkuu wa Ukaguzi wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) Mohd Shadhil amewashauri Wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa kutoka nje ya nchi kuacha kununua bidhaa zinakaribia kumaliza muda wa matumizi ili kujiepusha  kupata hasara isiyoyalazima.

Amesema kuna baadhi ya Wafanyabiashara wa Zanzibar huingiza bidhaa zikiwa zimebakia miezi michache kumaliza muda wa mutumizi kwa bei ndogo wakitegemea kupata faida kubwa wanapoziingiza Zanzibar.

Mkuu wa Ukaguzi wa ZFDA alieleza hayo wakati wa kazi ya kuteketeza zaidi ya tani 183 za bidhaa mbali mbali zilizoharibika na kupitwa na muda wa matumizi katika jaa la Kibele, Wilaya ya Kati.

Aliwahakikishia Wafanyabiashara kuwa ZFDA haina nia ya kuwatia hasara lakini na wao wanatakiwa wawe waangalifu zaidi na kuwahurumia wananchi wenzao wanaponunua bidhaa nje ya nchi.

Aidha Mohd Shadhil amewahimiza Wafanyabiashara wa Zanzibar kuhifadhi bidhaa zao katika maghala yaliyo rasmi na yenye sifa ya kuhifadhia ili ziweze kukaa muda mrefu bila kuharibika.

Alisema baadhi ya bidhaa  zilizoharibika na kumaliza muda wa matumizi ziligundulika katika zoezi la ukaguzi  lililofanywa na maafisa wa ZFDA bandarini Unguja  na katika maghali ya kuhifadhia bidhaa.

Bidhaa zilizoteketezwa ni mchele tani 163 uliofeli vipimo vya maabara na  uliongizwa nchini na Kampuni ya Zenj General Marchandize Ltd na unga wa ngano tani sita ulioharibika baada ya kuingia maji ya mvua.

Bidhaa nyengine ni tende tani tano, vipodozi tani moja, juice na bidhaa mchanganyiko vyote vikiwa vimemaliza muda wa matumizi ya binadamu.

Loading