WIZARA YA AFYA YATOA DAWA ZA KULINDA NGOZI YA WATU WENYE UALBINO

Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akimkabidhi Mkurugenzi wa Jumuiya ya Watu wenye ualbino Zanzibar Ussi Khamis dawa za kulinda ngozi kwa wanachama wa Jumuiya hiyo katika hafla iliyofanyika ofisini kwa waziri Mnazimmoja

Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashidi Mohamed ameitaka Jumuia ya Watu wenye ualbino Zanzibar kufanya uhakiki wa kina kujua taarifa ya watu wenye matatizo hayo ili kuja mahitaji sahihi ya dawa zinazohitajika.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya imeweka bajeti ya kutosha ya kununulia dawa kwa ajili ya wananchi wote bila malipo yakiwemo makundi maalum.

Waziri Hamad alieleza hayo Ofisini kwake Mnazimmoja wakati akikabidhi dawa za kulinda ngozi (lotion) kwa Jumuiya ya watu wenye ualbino Zanzibar.

Alisema iwapo Jumuiya ya Watu wenye ualbino itakuwa na taarifa sahihi ya wananchi wenye matatizo hayo itakuwa rahisi kuwapatia kinga na kuwapunguzia matatizo yanayowakabili.

Waziri wa Afya aliwataka viongozi wa Jumuiya kushirikiana na Kitengo cha elimu ya Afya kutoa elimu juu ya mahitaji na matatizo yanayowakabili na kuandaa programu ya mahitaji yao ili kupatiwa ufumbuzi wa haraka kabla ya kusababisha athari kubwa ikiwemo saratani ya ngozi.

Aliishauri Jumuiya hiyo kutekeleza majukumu yake kwa uwazi na uadilifu na kuhakikisha kwamba wanachama wake wote wanafaidika na wanatoa mawazo yao katika kuiimarisha.

Mkurugenzi wa Bohari Kuu ya Dawa Zanzibar Zahran Ali Hamad alisema watu wenye ualbino wamekuwa wakitumia fedha nyingi kununua dawa za kulinda ngozi na kuwepo kwa dawa hizo itakuwa msaada mkubwa kwao.

Alisema zaidi ya shilingi milioni 13 zimetumika kununulia vichupa 200 vya dawa ya kujipaka kwa watoto na watu wazima na utaratibu wa kununua dawa hizo utakuwa endelevu.

Akipokea sehemu ya dawa hizo Mkurugenzi wa Jumuiya ya Watu wenye ualbino Zanzibar Ussi Khamis Debe aliishukuru Wizara ya afya kwa kuwathamini na kuwapatia dawa hizo

Alimueleza Waziri wa Afya kuwa Jumuiya yao ilianzishwa mwaka 2009 na hadi kufikia sasa inawanachama 186 Unguja na Pemba wanafanya juhudi ya kuongeza wanachama.

Alisema baadhi ya watu wenye ualbino wamekuwa wakishindwa kununua dawa za kulinda ngozi kutokana na gharama kubwa na hatimae husababisha athari ya afya zao.

Alisema athari kubwa inayowapata watu wenye ualbino ni kupata saratani ya ngozi na tayari watu 16 waliopata maradhi hayo 11 wameshafariki.

Aliishauri Wizara ya Afya kuweka kliniki maalum ya watu wenye matatizo ya ualbino ili kuwapunguzia kukaa muda mrefu kusubiri dawa katika kliniki za kawaida ambapo baadhi ya wakati husumbuliwa na jua kali ambalo linaathiri afya zao.

Loading