ZANZIBAR KUADHIMISHA SIKU YA AFYA YA KINYWA NA MENO DUNIANI KESHO MACHI 20

Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akizungumza na wandishi wa habari (hawapo pichani) kuelekea maadhimisho ya siku ya Afya ya Kinywa na Meno Duniani yatayofanyika kesho tarehe 20/03/19 Mapinduzi Square Michenzani Mjini Unguja.

Zaidi ya asilimia 50 ya watoto wanaugua  maradhi ya kutoboka kwa meno jambo ambalo hupelekea kuathirika kwa kinywa na afya ya meno.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohammed wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na siku ya Afya ya Kinywa na Meno Duniani huko ofisini kwake Mnazi Mmoja.

Amesema jamii imekuwa ikiathirika na kutoboka kwa meno hasa watoto kutokana na kula vyakula vyenye sukari na kutofuata mambo muhimu katika kujikinga na usafi wa kinywa.

Amesema mabadiliko ya tabia na ulaji wa vyakula vya sukari kwa wingi ni ongezeko la maradhi ya kinywa na meno na kupelekea kuongezeka kwa kiasi kikubwa kutoboka kwa meno.

Alieleza kuwa ni muhimu kutunza afya ya kinywa ili kuepukana harufu mbaya ya kinywa na meno kutoboka kwa kujikinga na kupata matibabu kabla ya kuathirika zaidi.

“Maradhi haya ya kinywa na meno sio maradhi madogo ni maradhi makubwa duniani kwani maradhi haya husabisha kansa mbalimbali ni lazima kufanya kinga ya usafi na kuwaelimisha vijana na watoto skuli,” alifahamisha  Waziri Hamad.

Mkuu wa Madaktari wakujitolea kutoka Chuo Kikuu cha Belgrade Prof. Ana Pucar akielezea juu ya umuhimu wa kutoa elimu ya Afya ya kinywa na meno kwa watoto walio shuleni katika Mkutano wa Waziri wa Afya uliofanyika Ofisini kwake Mnazimmoja Mjini Zanzibar.

Aidha Waziri Hamad aitaka jamii kudhibiti ulaji wa vitu vya sukari mara kwa mara na kuboresha mbinu za upigaji mswaki kwa kutumia dawa ili kuweza kujikinga na maradhi hayo.

Waziri huyo wa Afya ameeleza kuwa serikali imekuwa ikitoa elimu juu ya uhifadhi na kinga ya kinywa na meno katika skuli mbalimbali mjini na vijijini  pamoja na kuboresha huduma za afya katika vituo kwa kuweka vifaa na wataalamu ili kuepukana na maradhi hayo.

Amewataka wananchi kuwa na utamaduni wa kufanya uchunguzi wa meno katika vituo vya afya angalau mara mbili kwa mwaka ili kuepukana na madhara ya kinywa na meno kwa lengo la kupata afya bora.

Waziri Hamad Ameeleza katika kudhimisha siku hiyo Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wataalamu wa meno kutoka   Chuo Kikuu cha Belgrade kesho inatarajia kutoa huduma mbalimbali za matibabu ya meno huko katika Mnara wa Kumbukumbu Kisonge.

Daktari bingwa wa meno Zanzibar Iddi Sleiman Iddi akijibu baadhi ya maswali yalioulizwa na wandishi wa habari katika kuelekea madhimisho ya Afya ya Kinywa na Meno Duniani.

Nae Daktari Bingwa wa Meno Idd Suleiman Idd amewasisitiza kinamama wajawazito kufika mapema katika vituo vya Afya  kupima afya ya kinywa na meno ili kuepuka madhara kwa mtoto.

Ameeleza kuwa madhara ya kinywa na meno kwa wajawazito huweza kumuathiri mtoto na kupelekea kuzaa watoto wasiotimia umri.

Siku ya Afya ya Kinywa na Meno Duniani  huadhishwa kila ifikapo tarehe 20  Machi ambapo ujumbe wa mwaka ni “Tunza Afya ya Kinywa”

Loading