Mtayarishaji wa kitabu cha maradhi ya njia ya mkoji Dk. Zhang Junjie akimkabidhi Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bi. Asha Ali Abdalla msaada wa kitabu pamoja na vifaa tiba (kushoto) Naibu Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China Zanzibar Shen Qi. hafla hiyo imefanyika Wizara ya Afya Mnazi mmoja.
Timu ya Madaktari wa Kichina wanaofanyakazi Hospitali Kuu ya Mnazi mmoja imeikabidhi msaada wa kitabu na Vifaa Tiba Wizara ya Afya Zanzibar kwa ajili ya matumizi ya Hospitali hiyo.
Mmoja wa Madaktari wa timu hiyo, mtayarishaji wa kitabu hicho Dk. Zhang Junjie alimkabidhi Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bi. Asha Ali Abdalla msaada huo katika hafla iliyofanyika Ofisini kwake Mnazi mmoja.
Dk. Zhang alisema msaada huo ni muendelezo wa ushirikiano wa miaka mingi uliopo baina ya Jamhuri ya Watu wa China na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha huduma za Afya.
Alikumbusha kuwa Jamhuri ya Watu wa China ilianzisha ushirikiano wa kuleta Madaktari Zanzibar tokea mwaka 1964 na utaratibu huo umekuwa ukiendelezwa na kuimarishwa zaidi hadi hivi sasa.
Alieleza matarajio yake kuwa msaada wa kitabu na vifaa tiba vilivyotolewa vitasaidia katika kuimarisha huduma za afya katika Hospitali ya Mnazimmoja na Hospitali nyengine za Zanzibar.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bi. Asha Ali Abdalla aliishukuru timu ya 28 ya Madaktari wa China kwa msaada wa vitabu ambavyo vitakuwa ni chanzo cha mafunzo kwa Madaktari wa Mnazimmoja.
Aidha alisema vifaa Tiba vitaongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa katika Hospitali hiyo ambayo bado inakabiliwa na changamoto ya Teknolojia na Rasilimaliwatu.
Mkurugenzi Kinga Dk. Fadhil Abdalla alisema kitabu walichokabidhiwa na Timu ya Madaktari wa China ambacho kinahusiana na matatizo ya maradhi ya njia za mkojo, ikiwemo tenzi dume, vitatumika kama muongozo na mapitio kwa madaktari wakati wa kufanya upasuaji.
Dk. Fadhil aliongeza kuwa kitabu hicho pia kitatumika kuwasomesha Madaktari wanafunzi wa Taasisi ya Sayansi za Afya ya Binadamu ya SUZA iliopo Mbweni ili kuelewa kwa undani tatizo la maradhi ya njia za mkojo na tiba yake.
Makabidhiano ya Kitabu na Vifaa vya Tiba yalihudhuriwa pia na Naibu Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China Zanzibar Shen Qi.