KITENGO CHA KINYWA NA MENO HOSPITALI YA MNAZI MMOJA CHATOA HUDUMA YA MENO KWA WATOTO WANAOLELEWA NYUMBA YA MAZIZINI.

Mkuu wa Kitengo cha Meno na Kinywa Hospitali ya Mnazi mmoja Dkt. Semeni Shaban Mohd akimfanyia uchunguzi wa meno Faiza Josef Lumelezi huko Mazizini.

Wizara ya Afya Zanzibar kupitia Kitengo cha Meno Hospitali Kuu ya Mnazi mmoja kimetoa elimu ya utunzaji na uchunguzi wa meno na kinywa kwa watoto wanaolelewa katika nyumba ya watoto Mazizini.

Mkuu wa Kitengo cha Meno na Kinywa Hospitali kuu ya Mnazi mmoja Dk. Semeni Shaban Mohd alisema zoezi la kuwafanyia uchunguzi watoto lilianza mwanzoni mwa wiki hii katika skuli mbali mbali za mjini na mashamba Unguja na Pemba.

Alisema kazi hiyo itaendelea hadi tarehe 20 mwezi huu siku ya kilele cha maadhimisho ya siku ya kinywa na meno duniani ambapo kwa Zanzibar itaadhimishwa katika Uwanja wa Mapinduzi Square Michenzani.

Aliwashauri wananchi kujitokeza katika maadhimisho hayo ambayo yataambatana na uchunguzi wa kinywa na meno watu wote watakaofika siku hiyo na watakaobanika kuwa na matatizo watapatiwa matibabu bila malipo.

Dk. Semeni Shaban Mohd aliwashauri wananchi kupunguza kula vyakula vyenye sukari mara kwa mara na kuacha tabia ya kuwapa vijana wao vyakula vyenye sukari nyingi wanapokwenda skuli kwani ni moja ya sababu ya kuharibika kwa meno na tatizo la vizi kwa vijana wengi .

Aidha aliwataka wananchi kupiga msuaki angalau mara tatu kwa siku na kuhakikisha wanatumia dawa ya meno yenye Chloride kwani inaweka ulinzi wa meno kutoboka na kukifanya kinywa kuwa katika afya nzuri.

Mdhamini wa kitu cha kulelea watoto yatima Mazizini Chumu Ali Abeid aliwashukuru madaktari wa Kitengo cha meno na kinywa Hospitali ya Mnazimmoja kuwafanyia uchunguzi watoto wanaolelewa katika nyumba hiyo.

Alisema elimu iliyotolewa na madaktari wa kitengo hicho wakati wa uchunguzi, limewasaidia kupata mafunzo juu ya njia bora ya kusafisha meno.

Alisema elimu waliyoipata wataitumia katika kuwasimamia watoto wapatao 30 wanaolelewa katika nyumba hiyo kuhakikisha wanafuata misingi bora wakati wa kupiga msuaki ili kulinda afya ya meno na kinywa.

Kaulimbiu ya siku ya kinywa na meno duniani mwaka huu ‘Tufanye mdomo uwe na afya bora.

Loading