Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya ziara maalum katika kitengo cha Watoto wanaosumbuliwa na maradhi ya Moyo Hospitali ya Mnazi mmoja Zanzibar.
Serikali ya Mpinduzi ya Zanzibar inatarajia kujenga Taasisi ya Kitengo cha Maradhi ya Moyo kata kijiji cha Binguni Wilaya ya Kati ili kupunguza gharama za matibabu ya maradhi hayo.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Muhamed wakati alipotembelea watoto wenye maradhi hayo huko katika Hospitali kuu ya Mnazimmoja.
Amesema gharama za matibabu ya maradhi hayo ni kubwa na yanapatikana nje ya nchi hivyo Serikali imeamua kujenga ili kuwaondoshea usumbufu Wananchi.
Aidha amesema Serikali itaendelea kuwapatia wananchi huduma bora za matibabu bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
Amesema uhusiano nzuri uliodumu kwa miaka 21 baina ya Zanzibar na Israil katika kutoa matibabau hivyo ni vyema kwa wananchi kuipokea huduma hiyo ili wafaidike kwani matibabu ya maradhi ya moyo ni makubwa ukilinganisha na hali za wananchi.
Aidha amefahamisha kuwa kwa kipindi hiki wataongeza vitanda 1000 kwa wagonjwa na kutoa mafunzo kwa Madaktari na Manesi wa Hospitali ya Mnazimmoja ili wananchi waweze kupata huduma bora zaidi kwa wagonjwa wa maradhi ya moyo.
Waziri Rashid ameongeza kuwa kwa mwaka huu wameanza matayarisho ya ujenzi wa jengo la maradhi ya moyo kwa kupeleka wataalamu katika eneo linalotakiwa kujengwa jengo hilo kwa ajili ya kuangalia mazingira.
Hata hivyo Waziri wa Afya amewasihi madakatari wanaopatiwa mafunzo hayo kuyatumia vizuri ili kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.

Kwa upande wa Daktari anaesimamia kitengo hicho Omar Mohamed Suleiman amesema kuwa kwa sasa wana wagonjwa 1800 ambao wapo waliobainika kuwa na maradhi hayo ambapo pia wapo wenye maradhi matibabu mbalimbali ya upasuaji.
Amesema kuwa kundi la mwanzo waliopatiwa matibabu Israel ni 550 na kila wanapokuja wataalamu hao wanawafatilia wale waliowafanyia upasuaji wa awali ili kudumishana ushirikiano kwa wagonjwa na wataalamu hao.
Aidha amefahamisha kuwa kwa muda wa siku nne wanatarajia kuwachunguza watoto 400 wenye matatizo ya moyo na wakigundulika kuna wana matatizo hayo na wanahitaji kufanyiwa upasuaji watafanya hatua ya kusafirishwa.
Hata hivyo amesema wanatarajia kutafuta wahisani kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kujua sababu halisi ambazo zinapelekea maradhi hayo.
Nao wazazi wenye watoto ambao wana maradhi ya moyo wamesema kuwa tatizo kubwa linalowakabili ni ukosefu wa wa fedha za kununua dawa pindi wanapokwenda Hospitali kushindwa kumiliki kutokana na hali ngumu ya maisha.
Aidha wameishukuru Serikali kwa kuwapatia huduma hiyo na kuwataka wazazi wenye watoto ambao wana maradhi ya moyo kufuata tarehe walizopangiwa kwa wakati ili kuondosha malalamiko kwa baadhi ya wagonjwa.