MKURUGENZI KINGA NA ELIMU YA AFYA AZUNGUMZA NA WAANDISHI ZANZIBAR.

Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dk,Fadhill Mohamed Abdalla akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na Tahadhari zilizochukuliwa kujikinga na Maradhi ya Corona yaliozuka katika Nchi ya China hafla iliofanyika Ofisini kwake Wizara ya Afya Mnazimmoja Zanzibar

Wananchi wametakiwa kufika katika Vituo vya Afya kwa ajili ya uchunguzi na kupatiwa matibabu mara watapobaini kuwa na mafua na homa kali ili kujikinga na maradhi ya Corona yaliyojitokeza nchini China hivi karibuni.

 Hayo yameeleza Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dkt Fadhil Mohamed Abdallah huko Ofisini kwake Wizara ya Afya Mnazimmoja wakati aliopokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na maradhi hayo.

Amesema dalili ya maradhi hayo ni kuhisi mafua na homa ambayo baadae huzidi hatimae kupata homa kali, vidonda vya mdomo na kwenye mishipa ya koo pamoja na homa ya mapafu.

Mkurugenzi huyo amewasisitiza wananchi kufuatia taarifa zinazotolewa katika vyombo vya habari kuhusiana na maradhi hayo ili kuepuka uzushi katika jamii na kuishi kwa amani kutokana na hali ya maradhi ilivyo nchini.

Dkt Fadhil amefahamisha kuwa kirusi cha maradhi hayo kipo toka zamani lakini kwa sasa kimezuka kirusi chengine kipya kinachoitwa Novel Corona Virus ambacho kinatokana na jamii hiyo na kinaenea kwa kutumia njia ya hewa.

 Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa wameongeza nguvu za ziada katika maeneo ya Uwanja wa Ndege na Bandarini kwa kuwapa mafunzo maafisa wa vitengo hivyo pamoja na kuweka vifaa maalum vya kutumia katika Hospitali ya Mnazi mmoja pindi yakigundulika maradhi hayo ili kuweza kudhibiti yasienee nchini.

“Lakini pia tumeandaa eneo maalum huko Fuoni Kibondeni  kwa ajili kuwaweka wagonjwa pindi tu tukigundua kuwa mgonjwa  amejitokeza na maradhi hayo, na pia tunatoa mafunzo katika  vituo vya afya jinsi ya kuhudumia wagonjwa na kutoa fomu maalum kwa wageni wote wanaotoka nchi ambazo zimegundulika kuwa na maradhi hayo na tutawafatilia kwa muda wa siku 14 ili kupata taarifa zake”, alisema Dkt Fadhil.

Amefahamisha kuwa Serikali imejipanga kwa ajili ya kujikinga na maradhi hayo tayari imeshaunda timu sita ili kufuatilia wagonjwa wanaopata maradhi hayo na kuwapatia mafunzo pamoja na kutoa taarifa mbalimbali kupitia vyombo vya habari kuhusu ugonjwa huo.

Akizungumzia kuhusu maradhi ya Malaria Dkt Fadhil amesema kuwa katika jamii kuna mbu wanaosababisha maradhi hayo  hivyo amewataka wananchi kuchua tahadhari kwa kuweka mazingira safi pamoja kutumia vyandarua vyenye dawa ili kujikinga na maradhi hayo.

Loading