ZANZIBAR YAPATIWA MSAADA WA MASHINE 17 ZA KUSAFISHIA FIGO

Kaimu Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania Ahmad Saleh Ghamdi akimkabidhi Waziri wa Afya Hamad Rashid Muhamed mashine za kusafishia Figo katika sherehe zilizofanyika Bohari Kuu ya Dawa Maruhubi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar

Serikali ya Saudi Arabia imetoa msaada wa mashine 17 za kusafishia Figo (Dialysis Machines) kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zenye thamani ya shilingi milioni 400.

Kaimu Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania Ahmed Saleh Ghamdi alimkabidhi Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Muhamed msaada huo katika hafla iliyofanyika Bohari Kuu ya Dawa Marughubi.

Kaimu Balozi Ahmed alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Muhamed Shein na Serikali yake kwa juhudi kubwa wanazochukua katika kuimarisha uchumi na sekta ya afya.

Alisema Serikali ya nchi yake itaendelea kuunga mkono juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa katika kukuza sekta ya afya na elimu ambazo ni muhimu katika kuimarisha ustawi wa wananchi.

Aliongeza kusema kuwa Serikali ya Saudi Arabia itafikiria kutoa nafasi za masomo kwa madaktari wa Zanzibar hasa katika fani ambazo bado zinaupungufu wa wataalamu ili ziweze kuimarika katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

Waziri wa Afya Hamad Rashidi Muhamed aliipongeza Serikali ya Saudi Arabia kwa misaada mbali mbali inayotoa kwa Zanzibar ikiwemo ya kuimarisha huduma za afya nchini.

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Hamza (kushoto) akiwa na Waziri wa Afya Hamad Rashidi na Naibu wake Harusi Suleiman na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Halima (kulia) wakiangali mashine za kusafishia Figo zilizotolewa na Serikali ya Saudia Arabia katia Bohari kuu ya Dawa Maruhubi.

Alisema mashine 17 za kusafishia Figo zilizotolewa na Serikali ya nchi hiyo zitawapunguzia na kuwarahisishia kazi watendaji na wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo kuipata kwa urahisi.

Aliongeza kuwa Zanzibar kama zilivyo nchi nyengine zinazoendelea, wagonjwa wa maradhi yasiyoambukiza ikiwemo matatizo ya Figo imekuwa ikiongezeka na kunahitajika kuongeza huduma za kuwahudumia wagonjwa wanaokabiliwa na matatizo hayo.

Alisema baada ya kupatikana msaada wa mashine hizo 17, Wizara itapeleka mashine 10 Pemba na inakusudia kuanzisha  huduma ya kusafisha Figo

katika hospitali nyengine za Unguja ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali kuu ya Mnazimmoja.

Msaidizi Muuguzi wa Kitengo cha Figo Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Zainab Ismail alisema kuongezeka kwa idadi ya mashine za kusafishia Figo katika Kitengo hicho kutawarahisishia utendaji wa kazi na wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo kuipata kwa haraka.

Alisema kazi ya kusafisha Figo huchukua karibu saa nne kwa mgonjwa mmoja na idadi ya wagonjwa waliopo Zanzibar hivi sasa ni wengi hivyo kulikuwa na umuhimu mkubwa kupata mashine nyengine kurahisisha utoaji wa huduma katika Kitengo hicho.

Loading