Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed akitoa hotuba katika hafla ya siku ya Wachangia Damu Duniani(WORLD BLOOD DONOR DAY)iliofanyika Uwanja wa Mwanakwerekwe Sokoni mjini Zanzibar.
Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed amewataka wananchi waongeze juhudi ya kuchangia damu ili kuokoa maisha kwa wagonjwa aliokuwa hatarini ambao wanahitajika kusaidiwa damu kutokana na matatizo mbali mbali.
Hayo aliyasema huko katika Uwanja wa Mwanakwerekwe Sokoni Wilaya ya Magharibi B Unguja wakati wa Sherehe ya Kuadhimisha siku ya uchangiaji damu duniani .
Alisema wananchi wenye moyo wa kuchangia damu kwa hiyari huokoa maisha ya watu wengi ambao wanahitaji huduma ya kusaidiwa damu wakiwemo mama wajawazito na waliojifungua ni zaidi ya asilimia 75 ,wahanga wa ajali pamoja na wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji .
“Damu ni uhai bila ya damu huna uhai huwezi kufanya kazi kama huna damu ya kutosha pia huwezi juwa wakati gani utapata tatizo. “alisema Waziri wa Afya
Aidha alisema ukaguzi unahitajika katika sehemu zote zinazohifadhiwa damu ili kuhakikisha damu iliyopo ipo katika hali ya usalama na inatumika ipasavyo bila ya kukaa hadi kuharibika.
Alifahamisha kuwa utowaji wa damu kwa wananchi kumesaidia kuepua matatizo mbali mbali ya Maradhi hasa magonjwa ya ini ambayo yameonekana kwa baadhi ya wananchi ambao walikuwa bado hawajajibaini na kuweza kupatiwa huduma za tiba mapema .
Alisema takwimu zinahitajika kwa kila wilaya kuweza kujuwa kiasi gani cha mahitaji ya damu ambayo yanahitajika ili kuweza kujipanga kwa mujibu wa mahitaji yaliopo.
Pia aliwashukuru wananchi kwa uwelewa wa kujitokeza katika kuchangia damu kwani kila siku mahitaji ya damu yanahitajika kuongezeka kutokana na ongezeko la idadi ya watu .
Hata hivyo alitoa shukurani kwa wananchi mbali mbali Jumuiya pamoja na Taasisi za Serikali ikiwemo Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Vikosi vya ulinzi na usalama,sehemu za ibada Msikitini pamoja na Kanisani.
Nae Mkuu wa Wilaya Magharibi B Kapteni Silima Haji Haji alipongeza jitihada zilizochukuliwa za uhamasishaji wananchi pamoja na jumuiya mbali mbali ili kujitokeza kwa wingi kwa kuitika wito huo wa kuchangia damu zao .
Aidha alisema kufanya hivyo ni kusaidia kuokoa maisha ya watu wengi ambao wanapata matatizo mbali mbali ya kiafya ikiwemo wahanga wa ajali .
Kaimu Meneja wa mpango wa damu salama Uchangiaji Omar Juma Kidawa alisema wataendelea kuwahamasisha wananchi katika sehemu mbali mbali ili hakikisha uchangiaji unaongezeka kulingana na mahitaji ya wananchi .
Alisema kila siku idadi ya wachangiaji inazidi kuongezeka kuanzia Januari mosi hadi sasa imeshapatikana damu unit 6954 jambo ambalo linatia moyo sana kila siku idadi inaengezeka ya uchangiaji kwa wananchi.
Meneja Mstaafu wa kuchangiaji damu Mwanakheir Mahamoud aliahidi kuwa sambamba katika kuhamasisha watu kuchangia damu kwani ni suala muhimu ambalo linaokoa wengi kwa kuweza kuchangiwa damu salama .
Katika Sherehe hiyo ya Uchangiaji Damu Duniani zawadi mbali mbali zimetolewa kwa Wananchi Jumuiya, Taasisi pamoja na Nyumba za Ibada kwa kuwa wachangiaji bora.