Uzinduzi wa Mpango shirikishi wa kutokomeza Kipindupindu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akikata Utepe wa Vitabu vya Mpango kama ishara ya Uzinduzi rasmi wa mpango shirikishi wa kutokomeza Kipindupindu Zanzibar katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Idris Abdulwakil

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, alisema serikali ina wajibu wa kuwatunza na kusimamia Afya za wananchi, kwa kuhakikisha wanaondokana na maradhi mbali mbali, ikiwemo kipindupindu .

Dk. Shein amesema hayo katika Uzinduzi wa Mpango shirikishi wa kutokomeza Kipindupindu, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakili, kikwajuni mjini hapa.

Alisema katika kufanikisha azma hiyo Serikali inaendelea kufanya juhudi za kuhakikisha huduma za maji safi na salama yanapatikana kwa uhakika nchini kote.

Alisema wananchi wa Zanzibar wanahitaji kupata maji yalio safi na salama ili kuondokana na kadhia ya ugonjwa wa kipindupindu, akibainisha chanzo cha ugonjwa huo kuwa kinatokana na uchafu wa mazingira, sambamba na matumizi ya maji yasio salama.

Alisema Serikali kwa kushirkiana na washirika wa maendeleo hivi sasa imekuwa ikitekeleza miradi mbali mbali ya upatikanaji wa maji safi na salama, ili kuimarisha afya za wananchi wake.

Aidha, alisema Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa misingi ya maji ya mvua na miundombinu ya maji machafu ili kuyawezesha maji ya mvua kupita, sambamba na ujenzi wa vyoo na karo katika makazi ya wananchi.

Loading