ELIMU YA MATUMIZI YA CHAKULA VINYWAJI KWA WANAFUNZI YATOLEWA ZANZIBAR

Mkuu wa kitengo cha Uchambuzi wa Athari zitokanazo na Chakula wa Wakala wa Chakula na Dawa (ZFDA)Aisha Suleiman akitoa Elimu ya Matumizi ya Chakula Vinywaji pamoja na Peremende kwa Wanafunzi wa Skuli ya Glorious Academy Mpendae mjini Zanzibar.

Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar imepiga marufuku kutumia bidhaa ambazo vifungashio vyake havina maandishi ya lugha iliyokubalika kutumika kisheria nchini.

Akitoa elimu kwa wanafunzi wa skuli ya Glorious Acedemy huko Mpendae kuhusiana na uvumi uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu pipi na chokleti zimeingia nchini kuwa zina madhara Mkuu wa Kitengo cha Uchambuzi wa athari zitokanazo na Chakula Aisha Suleiman amesema ni marufuku kutumia bidhaa kama pipi na chokleti ambazo maandishi yake yameandikwa kwa lugha isiyofahamika.

Amesema hakuna pipi ama chokleti zinazoingizwa nchini ambazo zina madhara wala athari kwa jamii bali ni kuzingatia vifungashio, viambata vilivyomo katika bidhaa na muda wa kumalizika kwake.Ameeleza Wakala wa Chakula na Dawa ina jukumu la kuhakikisha kwamba vyakula vinavyoingia nchini viko salama kwa matumizi ya binadamu na havileti madhara kwa mtumiaji.

Walimu pamoja na Wanafunzi wa Skuli ya Glorious Academy wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa kitengo cha Uchambuzi wa Athari zitokanazo na Chakula wa Wakala wa Chakula na Dawa (ZFPA)Aisha Suleiman wakati akitoa Elimu ya Matumizi ya Chakula Vinywaji pamoja na Peremende kwa Wanafunzi wa Skuli ya Glorious Academy Mpendae mjini Zanzibar.

Mkuu huyo amewafahamisha wanafunzi hao kuwa waangalifu wanaponunua bidhaa zenye vifungashio kwa kuangalia vyema maelezo yaliyomo ili kuepuka kupata madhara. Aidha Mkuu huyo amewataka wanafunzi hao kuacha kutumia vyakula vyenye sukari kwa wingi ili kuepukana na maradhi mbali mbali na kupata taifa lililoimara.

Aidha amesisitiza wanafunzi hao kutosikiliza taarifa za uvumi uliopo na kuwa walimu kwa wenzao ili jamii iondokane na jambo hilo. Nao wanafunzi hao wamesema kuwa wataitumia vyema elimu waliyoipata na kuwa walimu wazuri kwa wenzao.

Loading