WAZIRI WA AFYA ZANZIBAR AWATAKA WANANCHI KUCHUKUWA TAHADHARI ZAIDI KUKABILIANA NA MARADHI YA CORONA

Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed akiwa na Msaidizi Meneja Programu ya Ukimwi, Homa ya Ini, Kifua Kikuu na Ukoma Issa Abeid Mussa wakionyesha ujumbe wa madhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani huko Wizara ya Afya wakati wa mkutano wa wandishi wa habari.

Wananchi wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari zaidi ya kinga katika kukabiliana na maradhi ya Corona ikiwemo kupunguza mikusanyiko na safari zisizokuwa za lazima.

Waziri Afya Hamad Rashid Mohamed alieleza hayo alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu hatua mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali kukabiliana na maradhi hayo.

Alisema ni vyema wananchi ambao hawana ulazima wakutoka, kubaki majumbani mwao na kujenga tabia ya kukosha mikono kila baada ya saa moja.

Waziri Hamada alisema kuwa Serikali imejipanga na kusisitiza kuwa wageni wote watakaoingia Zanzibar watawekwa karantini kwa kipindi cha wiki mbili kwa kujilipia gharama wenyewe.

Aliwashauri wazanzibari waliopo nje ya Zanzibar waendelee kubaki katika nchi waliko na watakapoamua kuja nchini watapelekwa katika kambi za karantini kwa wiki mbili.

Hata hivyo Waziri wa Afya aliweka wazi kuwa hadi sasa mgonjwa wa Corona aliegundulika Zanzibar bado ni mmoja na anaendelea na matibabu kwenye kituo cha Kidimni.

Aliwataka wananchi kukubali utaratibu uliowekwa na Serikali wa kupunguza msongamano katika Hospitali ya Mnazimmoja kwa kutoa nafasi watu wawili tu kuangali mgonjwa mmoja.

 Wakati huo huo Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed aliwataka wananchi, taasisi za Serikali na asasi za kiraia kuelewa kwamba maradhi ya kifua kikuu bado ni tatizo na ni miongoni mwa maradhi 10 yanyaoongoza kwa vifo duniani.

Akizungumzia siku ya maadhimisho ya Kifua kikuu duniani katika mkutano huo, Waziri Hamad alisema mwaka 2018 watu milioni 10 waligundulika na ugonjwa huo na milioni saba kati yao ndio waliofikiwa na huduma za matibabu na milioni 1.5 walifariki.

Kwa upande wa Zanzibar, mwaka 2019 wagonjwa 967 wa Kifua Kikuu waligundulika na kupatiwa matibabu ambapo 39 walifariki ikiwa ni sawa na asilimia nne.

Alizitaja dalili za maradhi ya kifua kikuu kuwa ni kukohoa kwa wiki mbili au zaidi, kupata makohozi yaliyochanganyika na damu, homa wakati wa jioni kutokwa na jasho jingi  hasa wakati usiku, kukonda na kupungua uzito.

Aliwataka wananchi watakaojiona na dalili hizo kuwahi mapema kwenye vituo vya afya kwani maradhi ya kifua kikuu yanatibika.

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya siku ya Kifua kikuu duniani mwaka huu ni Wakati ni huu ”Paza sauti zungumzia TB”.

Loading